Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza orodha ya pili ya wanafunzi waliofanikiwa kupata mikopo kwa mwaka wa masomo 2024/2025. Hii ni habari njema kwa wale wanaosubiri majina yao baada ya awamu ya kwanza kutangazwa mapema mwaka huu.
Makundi ya Wanufaika wa Mikopo Awamu ya Pili
Orodha ya pili inajumuisha wanafunzi wa shahada ya awali (Bachelor’s Degree) na stashahada (Diploma) waliojiunga na vyuo vikuu na vyuo vya kati nchini Tanzania. Jumla ya wanafunzi 30,311 wa shahada ya awali wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 93.7 bilioni. Hadi sasa, jumla ya wanafunzi 51,645 wamepata mikopo kwa mwaka huu wa masomo kupitia awamu ya kwanza na ya pili, na gharama ya mikopo yote ni TZS 163.8 bilioni.
Pia, wanafunzi wapatao 2,157 wa stashahada wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 5.6 bilioni, na wanafunzi 45 wa shahada ya uzamili (Master’s Degree) wamepangiwa mikopo yenye thamani ya TZS 205.6 milioni. Aidha, wanafunzi 16 wa shahada ya uzamivu (PhD) wamepangiwa mikopo ya jumla ya TZS 215.6 milioni.
Wanafunzi wa Samia Scholarship
Katika kundi hili, wanafunzi 588 wamefanikiwa kupata ufadhili kupitia Samia Scholarship, mpango maalum unaoendeshwa na serikali.
Kuendelea kwa Orodha ya Waliopata Mkopo Awamu ya Tatu
HESLB inaendelea kupokea taarifa za udahili na kuandaa orodha ya awamu ya tatu, ambayo itatangazwa hivi karibuni. Hii itahakikisha wanafunzi wote waliopangiwa mikopo wanaweza kuendelea na taratibu za kujisajili kwenye vyuo walikodahiliwa.
Jinsi ya Kuangalia Majina Yako
Ili kuangalia kama umefanikiwa kupata mkopo kupitia awamu ya pili, unaweza kutembelea tovuti rasmi ya HESLB na kufuatilia orodha ya majina yaliyochapishwa.
Post a Comment